Copyright © Tuombe | Theme by Dzignine | Customized and Installed by FanyaICT Solutions
Wednesday, January 29, 2014

Kunena kwa Lugha (1Kor 14:5a)

Moja ya vitu vinavyozua maswali mengi kati ya Wakristo, walioko kwenye neema ya wokovu na ambao bado hawajaingia ni karama ya kunena kwa lugha. Hii haishangazi sana kwa kuwa hata kwa Wakristo wa kwanza hali ilikuwa ni hivyo hivyo, kitu kilichomlazimu mtume Paulo kuandika sura nzima ya 14 ya waraka wake wa kwanza kwa kanisa la Korintho kuizungumzia kwa upekee akiilinganisha na karama ya unabii.
Kupitia sura hii (1Kor 14) na maeneo mengine ya Biblia tunajifunza kuwa kuna jinsi mbili karama hii inatenda kazi :
  1. Kunena kwa lugha kusiko na tafsiri
  2. Kunena kwa lugha kuliko na tafsiri 
Jinsi ya hii ya pili pia imegawanyika katika aina mbili
  • Lugha ya kibinadamu (Mdo 2:4-11)
Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, 
10 Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, 11 Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu. 
  • Lugha isiyo ya kibinadamu (1Kor 14:2,13)
Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake. 13 Kwa sababu hiyo yeye anenaye kwa lugha na aombe apewe kufasiri.
Lengo la mada hii ni kuizungumzia jinsi ya kwanza : Kunena kwa lugha kusiko na tafsiri.

Tunaposoma 1Kor 14:5a ;
Nami nataka ninyi nyote mnene kwa lugha, lakini zaidi sana mpate kuhutubu, ...
tunaona mtume Paulo anataka mambo mawili katika kanisa la Korintho : Kunena kwa lugha na kuhutubu (kutoa unabii) ; jambo la pili akilitaka zaidi kuliko la kwanza. Hii haiondoi ukweli kwamba jambo la kwanza pia analitaka katika kanisa hili.
Anazidi kuthibitisha zaidi ukweli huu katika mstari wa 18 wa sura hii ya 14 (1Kor 14 : 18),
Namshukuru Mungu ya kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote; 
yeye ambaye sura tatu nyuma (1Kor 11 : 1) tunakutana na agizo lake kwamba
Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo.
Lakini kwa nini hasa tunene kwa lugha ?

  • Kujijenga nafsi (1Kor 14 : 4a)
Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; . . .
Neno lililotumika kwa ajili ya 'kujenga' katika tafsiri ya Kiingereza ni 'to edify'. Neno la Kigiriki (lugha asili iliyotumika kuandika waraka huu) ambalo limetafsiriwa kwa neno la Kiingereza 'edify', pia linatafsirika 'to charge' yenye maana sawa na ile ya kuchaji betri !
Kwa hiyo tunaposema kujijenga nafsi, pia tunamaanisha kujiongezea nguvu za rohoni mithili betri inavyoongezewa nguvu kwa kuchajiwa. Kwa hiyo ukihisi kuishiwa nguvu za rohoni unaweza kujichaji kwa kunena kwa lugha !
  • Kuomba yale tunayopaswa kuyaomba lakini hatuyajui (Rum 8 : 26)
 Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. 
Kuna kipindi katika maisha yetu ya maombi huwa tunapata msukumo/mzigo wa kuomba lakini tukiwa hatujui tunachopaswa kuomba/kuombea na jinsi tunavyopaswa kuomba. Kupitia kunena kwa lugha Roho Mtakatifu hutusaidia kuomba ndani mwetu kwa kuwa Yeye anajua tupaswacho kuomba/kuombea.
  • Kuomba kadiri ya mapenzi ya Mungu (Rum 8 : 26, 27)
26 Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. 27 Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu
 Kupitia kunena kwa lugha tunapojiachilia kwa Roho Mtakatifu tunaweza kuomba tukiwa na uhakika wa asilimia zote kwamba ni kadiri ya mapenzi ya Mungu.
  • Kuomba wakati tunajishughulisha na mambo mengine (1Kor 14 : 14)
 Maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda.
Kupitia kunena kwa lugha tunaweza kuomba hata wakati tunafanya kazi nyingine ; kwa hiyo kuweza kutimiza agizo la Mungu la kuomba kila wakati kwa kuwa tunaponena kwa lugha ni roho inayoomba lakini akili haifanyi kazi.
  • Inatusaidia kutambua uwepo wa Roho Mtakatifu katika maisha yetu (1Kor 6 : 19)
 Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; 
Kadiri tunavyozidi kuwa na mazoea ya kunena kwa lugha ndivyo tunavyoizoeza miili na nafsi zetu kuutambua uwepo wa Roho Mtakatifu ndani yetu na kuwa na usikivu (sensitivity) na utii kwake. Pia hali hii inatusaidia kutambua dhambi na mazingira yake kwa haraka zaidi, maana mara nyingi huwa tunatenda dhambi pale  tunapokuwa hatuuoni uwepo wa Mungu katika maisha yetu.
  • Kumwadhimisha Mungu (Mdo 10 : 46)
 Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. . . .
Katika kumsifu, kumwabudu ama kumshukuru Mungu kuna kipindi huwa inafikia unataka kuendelea lakini unakosa maneno ambayo yanaweza kuelezea kile unachojisikia kumweleza. Hii inatokana na udhaifu wa kibinadamu wa lugha zetu. Katika hali hii kunena kwa lugha kunaweza kukusaidia kuelezea hisia zako mbele za Mungu kwa ukamilifu.

Kuna sababu zaidi ya hizi chache nilizozitoa za mimi na wewe kuhitaji karama hii ya kunena kwa lugha katika maisha yetu ya Kikristo, na zaidi sana ya maombi ; ukiendelea kusoma Biblia kwa mtazamo wa kuzitafuta na pia kumwomba Roho Mtakatifu akufunulie, kwa hakika utakutana nazo.
Ni matamanio yangu makubwa kwamba mada hii ikusaidie kama hauna karama hii ya kunena kwa lugha kuanza kuitamani na kumwomba Roho Mtakatifu anayegawa karama akujalie uipate kwa kuwa kupitia mtume Paulo aliyekuwa akiongozwa na Roho Mtakatifu tunajua Mungu anatamani kila Mkristo awe nayo (1Kor 14 : 5a).
Pia kama una karama hii, natamani mada hii ikusaidie kuona umuhimu wa kuitumia zaidi na zaidi. Kwa kufanya hivi, kama karama nyingine yoyote itakua na kukusaidia wewe pia kukua katika kuhusiana na Mungu.
Mtume Paulo anahitimisha sura ya 14 ya waraka wake wa kwanza kwa kanisa la Korintho (1Kor 14 : 39,40) kwa kusema
39 Kwa ajili ya hayo, ndugu, takeni sana kuhutubu, wala msizuie kunena kwa lugha. 40 Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu. 
Mungu Akutie nguvu za kutembea katika utakatifu na kukua katika kuhusiana Naye !

0 responses:

Post a Comment